DAWA ZA VIUAWADUDU KATIKA PAMBA KUPELEKWA IGUNGA NA NZEGA.
- Rehema Lucas
- Dec 14, 2017
- 1 min read

Bodi ya Pamba Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni za usambazaji mbegu na dawa za kuua wadudu waharibifu zinatarajia kuanza kupeleka jumla ya chupa 55,000 za dawa zitakazo saidia kuua wadudu wahalibifu katika Wilaya ya Igunga na Nzega mapema wiki ijayo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkaguzi wa Pamba wa wilaya ya Igunga George Kihimbi wakati akijibu swali la Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliyetaka kujua dawa hizo zitaanza kusambazwa kwa wakulima lini.
Alisema kuwa dawa hizo zinaweza kuhudumia ekari 55,000 za pamba katika maeneo yanayolima pamba, Igunga na Nzega ili kuhakikisha mimea hiyo haishambuliwi na wadudu waharibifu.
Kihimbi alisema kuwa zoezi hilo litakwenda sambamba na usambazaji wa bomba 1,000 za kupulizia dawa kwa ajili ya kukabiliana na wadudu ambao wameanza kukata mimea ya wakulima.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri alisema kuwa kitendo cha uchelewaji wa dawa za kuua wadudu kuwafikia wakulima kinaweza kusababisha mavuno hafifu na hasara kwa wakulima na hivyo kuwavunja baadhi yao moyo.
Alisema kuwa njia pekee ya kuwasaidia wakulima ni pamoja na kuhakikisha dawa zinawafikia wakulima kwa wakati kama walivyofanya katika mbegu ili kuepuka mazao yao kuharibika na kupata hasara.
Comments