WAZIRI MPINA AFUTA TOZO ZA MIFUGO ZINAZOTOZWA KINYUME NA SHERIA
- Rehema Lucas
- Dec 11, 2017
- 3 min read

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amefuta tozo ya faini ya shilingi elfu hamsini kwa kila Ng’ombe mmoja na ameuagiza Uongozi wa Wilaya ya Singida kuwarudishia mara moja fedha wafugaji wote waliotozwa faini kinyume cha Sheria katika zoezi la kukamata mifugo linaloendelea katika Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori.
Waziri Mpina ametoa maelekezo hayo leo alipotembelea eneo la Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori, kwenye Kijiji cha Handa na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma kupitia kwa Wakuu wa Wilaya ya Singida na Chemba kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo kufika katika eneo hilo kabla ya tarehe15/12/2017 kushughulikia mipaka baina ya eneo la Singida na Handa kwa upande wa Wilaya ya Chemba na migogoro ya wafugaji inayoendelea.
Waziri Mpina alisema utozaji wa faini wa shilingi 50,000/= toka shilingi 20,000/= za awali kwa kila Ng’ombe aliyekamatwa na shilingi 25,000/= kwa Mbuzi toka shilingi 5,000/= za awali haukubaliki na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Singida, Elias Tarimo kurudisha shilingi 30,000/= kwa kila Ng’ombe ambazo zimetozwa bila kufuata Sheria yoyote.
Baadhi ya wafugaji waliofika katika kijiji cha Handa kulalamikia tozo ya shilingi 50,000 kwa kila Ng’ombe mmoja walizotozwa na Halimashauri ya Wilaya ya Singida ni pamoja na Jerumani Waline aliyetozwa jumla ya shilingi 2,500,000/=, kwa idadi ya mifugo 66, Mabula Mwala aliyetozwa shilingi 1,950,000/= kwa idadi ya mifugo 45, Joel Tahan aliyetozwa jumla ya shilingi 1,000,000/= kwa idadi ya mifugo 31, Elizabeth Hamisi aliyetozwa shilingi 1,050,000/= kwa idadi ya mifugo 34,na Elizabethi Nyambi aliyetozwa jumla ya shilingi 350,000/= kwa idadi ya mifugo 8.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji bwana Jerumani Waline, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni kuainishwa kwa mipaka ya Kijiji cha Handa na Hifadhi ya Msitu wa jamii wa Mgori na eneo la kunyeshea maji mifugo ambapo alimuomba Waziri kulishughulikia suala hilo.
Waziri Mpina ameiagiza Halmashauri ya Singida kupitia mara moja tozo hizo na kuzipeleka kwenye Mamlaka husika ili zipitishwe na kuanza kutumika kwa taratibu zinazokubalika kisheria.
Pia amezitaka Halimashauri zote nchini kutojiingiza katika mtego wa kutoza faini ambazo hazipo kisheria kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuagiza kuwa kuanzia sasa Halimashauri zote zinatakiwa kutoa taarifa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pindi zinapotaka kuendesha operesheni za mifugo ili kuwa na ufahamu wa pamoja baina ya Wizara na wadau wengine hali ambayo itasaidia kuboresha operesheni hizo na kuondoa migongano isiyo ya lazima.
Aidha amewataka Watendaji kuwa makini wanaposhughulikia masuala ya mifugo kwa kuhusisha Sheria mbalimbali za Sekta ya Mifugo ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima kwa vyombo vya Serikali na kutolea mfano wa Uongozi wa Pori la Akiba la Swaga Swaga ulivyowazuia Wakaguzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia afya za mifugo iliyokamatwa katika pori hilo, akasisitiza kuwa ni ukiukwaji wa sheria kwa kuwa sheria namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003, kipengele 26 (a)1 kinawapa uwezo Wakaguzi kuingia na kuchunguza hali ya mifugo mahali popote ili kuona afya za mifugo.
Alizitaja baadhi ya Sheria za Mifugo ambazo ni muhimu kuzizingatia wakati wa operesheni za mifugo kuwa ni pamoja na Sheria ya Veternari Namba 16 ya Mwaka 2003, Sheria ya Tasnia ya Maziwa Namba 8 ya Mwaka 2004, Sheria ya Tasnia ya Nyama Namba 10 ya Mwaka 2006, Sheria ya Biashara ya Ngozi (The Hides, Skin and Leather trade Act) Namba 18 ya Mwaka 2008, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo Namba 12 ya Mwaka 2010.
Sheria nyingine ni Sheria ya Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo Namba 13 ya Mwaka 2010, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo namba 4 ya Mwaka 2012.
Akizungumzia ugomvi wa wafugaji kuingiza mifugo katika Pori la Akiba la Swaga Swaga na Msitu wa Jamii wa Mgori, Waziri Mpina amesema Viongozi wa Wilaya wanajukumu la kuyalinda maeneo hayo na wafugaji kuheshimu sheria za nchi.
Comments