top of page

WANAFUNZI 11,000 WAKOSA NAFASI ZA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA

  • Rehema Lucas
  • Dec 8, 2017
  • 2 min read

Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais (Tamisemi) Mh.Selemani Jafo (picha na maktaba)

Jumla ya wanafunzi 11,173 ambao ni asilimia 1.7 ya waliofaulu katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu, hawakuchaguliwa katika chaguo la kwanza la kujiunga kidato cha kwanza 2018.

Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 662,035 ambayo ni sawa na asilimia 72.75 ya wanafunzi waliokuwa wamefanya mitihani wa kumaliza darasa la saba na kufaulu, lakini 650,862 sawa na asilimia 98.31 ndiyo waliochaguliwa awamu ya kwanza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alitangaza jana kuwa hali hiyo inatokana na ufinyu wa madarasa uliopo katika halmashauri nyingi nchini.

Kutokana na sababu hiyo, Jafo ametoa wiki moja kuanzia siku ya kufungua shule kwa halmashauri kuhakikisha zinakamilisha miundombinu ili wanafunzi hao waweze kuanza masomo mara moja.

Katika taarifa yake, Jafo amesema mikoa ya Kusini inaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi ambao licha ya kufaulu vizuri, hawakuchaguliwa kujiunga na shule katika chaguo la kwanza.

Halmashauri inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliokosa nafasi ni Mbarali yenye jumla ya wanafunzi 1,578 ikifuatiwa na Halmashauri ya Sumbawanga 1,553, Nkasi 1,318 huku Wilaya ya Chunya ikiwa na idadi ndogo zaidi ya wanafunzi 80.

Halmashauri nyingine zilizoshindwa kuchukua wanafunzi wa chaguo la kwanza ni Lindi (170), Wilaya ya Mbeya (207), Jiji la Mbeya (1,227), Babati (581), Hanang’ (687), Wilaya ya Mpanda (262), Nsimbo (714), Bariadi (369) na Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambayo wanafunzi 1,207 walikosa nafasi pia.

“Nimeshatoa maelekezo kwa mikoa yote nchini kuwa inapaswa kukamilisha miundombinu hiyo ili wanafunzi watakaochaguliwa awamu ya pili waweze kuripoti shuleni kabla ya Februari 15,” alisema Jafo.

Waziri huyo alisema wanafunzi 1,912 wenye mahitaji maalumu ambao walifanya mtihani na kuchaguliwa, wote wamepata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza.

Aliwaagiza maofisa elimu mikoa na wilaya kote nchini kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaripoti shuleni Januari 8 mwakani na watakaoshindwa kufanya hivyo ndani ya wiki moja nafasi zao zitachukuliwa na watu wengine.


Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page