top of page

POLISI KUPEKUA KILA ‘GESTI’ DODOMA.

  • Khalidi
  • Dec 5, 2017
  • 2 min read

Katika kuelekea miaka 56 ya Uhuru, Jeshi la polisi mkoani Dododma limejipanga kufanya upekuzi katika nyumba za kulala wageni kama moja ya njia za kuimarisha ulinzi na kukabiliana na vitendo vya uharifu.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto alisema Dodoma inaendelea kupokea wageni wengi wanaofika katika harakati za ujio wa serikali na kwaajili ya sherehe hizo.

“Ujio huo wa wageni tunatambua kuwa kuna wahalifu wanaojipenyeza,” alisema kamanda Muroto, hivyo “Tumejipanga vyema kuhakikisha kuwa amani na utulivu unakuwepo wakati wote.

“Uharifu hautapata nafasi kipindi hiki kwani tunafanya msako mkali muda wote, mchana na usiku.”

Kamanda huyo alisema katika kuhakikisha mkoa huo unakuwa shwari watafanya upekuzi katika nyumba za kulala wageni, pia nyumba bubu zinazolaza wageni na wengi wao ni wahalifu zitafikiwa.

“Tutafanya upekuzi wa kushtukiza kwenye vyombo vya usafiri vinavyongia na kutoka Dodoma,” alisema zaidi kamanda huyo. Aidha, Muroto alisema polisi imeongeza nguvu za kuhakikisha usalama unakuwepo kwa kushirikiana na kampuni binafsi za ulinzi, mgambo na vikundi 67 vya polisi jamii vyenye mafunzo maalumu.

Mbali na hilo, alisema pia watashirikiana na mabaraza ya ulinzi na usalama ya mtaa kuhakikisha hakuna uharifu katika mitaa yao na kila eneo linakuwa salama.

“Tutafanya doria za miguu, pikipiki, magari na ulinzi katika maeneo nyeti pamoja na maeneo ya biashara na huduma kwa Umma,” alisema Muroto.

Aliwatahadharisha wote wanokuja Dodoma kufanya uharifu kuwa sio sehemu sahihi kwao na kwamba ni bora wasifike kabisa kwani hawatauwa salama.

Kamanda huyo pia alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma kuwa watulivu, kufanya shughuri zao kwa kufuata sheria na kuwafichua wahalifu katika kipindi hichi kinachoambatana na shamrashamra nyingi.

“Watu wema ni wengi kuliko wahalifu, tukiungana kufichua waharifu Dodoma yetu itabaki salama.”

Katika hatua nyingine, Kamanda Mroto alisema watu watatu wamekamatwa kwa wizi wa mali za wafanyabiashara katika zoezi la kubomoa vibanda vya biashara visivyo rasmi eneo la Railway.

“Zoezi kwa ujumla linaendelea na linasimamiwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama na ubomoaji unalenga kupanua ujenzi wa miundombinu ya reli baada ya eneo hilo kuvamiwa na wafanyabiashara,” alisema Muroto.

Comments


Top Stories

Join our mailing list

Never miss an update

© 2017 Fahari News 

bottom of page