SERIKALI YARAHISISHA ULIPAJI WA KODI YA ARDHI SASA NI KWA MTANDAO
- Admin
- Sep 7, 2017
- 1 min read

IMEELEZA kuwa mfumo mpya wa ukusanyaji kodi ya ardhi wa GEPG utasaidia kuepusha mlolongo kwa walipaji na kuondoa usumbufu kwa wananchi tofauti na mfumo uliokuwepo awali.
Aidha Mfumo huo pia umetajwa kuwa na faida zaidi kwakuwa utarahisisha utendaji kazi kwa Maafisa watakaohusika na ukusanyaji wa kodi ya ardhi kwa wananchi.
Hayo yalibainishwa na Afisa Tehama kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Liberath Mtawale wakati wa mafunzo ya Mfumo wa GEPG kwa wataalamu wa ukusanyaji kodi za serikali katika taasisi mbalimbali yaliyofanyika ofisi ya Msajiri wa Ardhi kanda ya nyanda za juu kusini jijini Mbeya.
Mtawale alisema miongoni mwa faida zitakazo patikana ni pamoja na kudhibiti mianya ya mazungumzo baina ya Mtoa huduma na mwananchi ambayo yalikuwa yakitoa mianya ya rushwa baina ya pande hizo mbili.
Alisema Faida nyingine ni kumpunguzia mwananchi muda wa kushughulikia ulipiaji kodi husika kwakuwa mfumo mpya utamwezesha kulipia hata kwa kutumia njia za kielektroniki ikiwemo simu za kiganjani.
Alisema simu zitakazotumia sio Smatphone pekee,bali hata simu ya kitochi ataweza kulipia au kuona taaarifa zake pasipo kufika ofisi za Ardhi.
Kwa upande wake Msajiri msaidizi Ofisi za Ardhi kanda ya nyanda za juu kusini, Magreth Mapunda alisema mfumo huo mpya hauna mkanganyiko tofauti na awali ambapo walilazimika kufanya kazi kwa kukadiria na kuongeza kuwa wateja pia wataufurahia.
Alisema pia kutokana na mfumo huo mpya Serikali itaweza kukusanya fedha nyingi kwakuwa hakutafanyika tena ujanja ujanja katika ukusanyaji wa mapato.
Naye Afisa Ardhi Kanda ambaye pia ni kaimu Kamishna wa Ardhi kanda,Msafiri Mmasi alisema mfumo wa GEPG utawezesha kuondoa malalamiko na tuhuma za rushwa kwa maafisa wa Ardhi huku akisema sasa kodi ya serikali itakusanywa kwa wakati.
Comments